Nabii Anayekanyaga Waumini Aibua Taharuki


TUNAAMBIWA kwenye vitabu vitakatifu kuwa, katika siku za mwisho kutakuwa na nyakati za hatari mno, tena zilizo ngumu kushughulika nazo.
Pia inaelezwa kuwa, katika siku za mwisho, hali ya kiroho na mwenendo wa wanadamu utakuwa mbaya mno kwani wataibuka manabii wa uongo na mafundisho ya namnanamna ya kupotosha wanadamu.

Hicho ndicho kinachotokea katika nyakati hizi ambapo ukimwacha yule mchungaji mwanamke, Diana Bundala anayejiita Mfalme Zumaridi au Mungu wa Duniani wa jijini Mwanza aliyefungiwa kanisa lake na Serikali hivi karibuni, mwingine ametoa kali ya mwaka.
Mfalme Zumaridi alikuwa akifanya ibada ya kuwakanyaga na kupita juu ya waumini wake waliolala kifudifudi wakimsujudia kama mungu wao.

SASA NABII BETHANIA
Achana na Zumaridi, yupo Nabii Bethania Simon ambaye ni mchungaji wa Kanisa la Neema ya Kitume (AMG) lililopo Mbezi- Luis jijini Dar, ambaye amekuwa akizua taharuki kwa mafundisho yake ya kukanyaga waumini na kubebwa mgongoni kama mtoto mdogo aliyepewa jina la Mchungaji Mkanyaga Watu.

AIBUKA NA STAILI MPYA YA MAOMBI
Safari hii, ishu siyo kukanyaga watu au kubebwa mgongoni jambo ambalo linalaaniwa na watu wa haki za binadamu, bali Nabii Bethania ameibuka na staili mpya ya maombi na uponyaji inayoshangaza wengi.
Nabii Bethania ambaye picha nyingi mitandaoni zinamuonesha akihubiri huku akiwa amewakanyaga waumini migongoni na nyingine akiwa amebebwa mithili ya mtoto mdogo, sasa amekuwa gumzo kufuatia kutumia jiwe la ajabu kuponya watu kanisani kwake.

Mbali na kutumia jiwe hilo ambalo baadhi ya watu wanadai ni ushirikina, pia amekuja na staili nyingine ya kuponya wagonjwa wa magonjwa sugu kama Ukimwi kwa kutumia pipi.
Nabii Bethania kwa sasa anajiita Jiwe la Mungu kwa kile alichodai kuwa ndilo jina alilopewa na Mungu na ndilo analolitumia na kuzua gumzo kubwa.


RISASI NA NABII
Kufuatia gumzo hilo, Gazeti la Risasi Jumamosi lilifika kanisani ambapo lilipata fursa ya kuzungumza na Nabii Bethania;
Mchungaji huyo anafunguka kuwa, alipata wito wa kwenda katika Mlima Duluti uliopo mkoani Arusha ambako huko alilala siku 7 kwenye mwamba mkubwa.
Nabii Bethania anadai kuwa, kwenye mwamba huo hapakuwa na mawe madogomadogo na alipoamka siku ya saba asubuhi alishangaa kukuta mawe saba madogomadogo pembeni mwake.

ASIKIA SAUTI
Anasema kuwa, baada ya kukuta mawe hayo, moja lilikuwa sehemu ya kichwani kwake ndipo akasikia sauti ikimwambia; “Hili ni jiwe la Mungu, watu walishike na uwagusishe kifuani mwao, nao wataponywa na shida zao zote.”

Anasema mbali na maelekezo hayo ya jiwe hilo, pia sauti hiyo ilimwagiza awape watu pipi maalum ambapo amekuwa akigawa mbilimbili kwa waumini wake, moja wanakula papo kwa hapo madhabahuni na nyingine mhusika anakula asubuhi kabla ya kula chochote.
“Kazi ya pipi maalum ni kufungua milango ya neema na baraka,” anasema Nabii Bethania.


TURUDI KWENYE JIWE
Mchungaji huyo aliendelea kufafanua juu ya jiwe hilo kuwa, ni jiwe maalum la kutumia wakati wa kuombea watu wenye shida zote duniani.

“Ndipo Mungu aliponiambia kuwa nitaponya watu wenye Ukimwi, kisukari, BP (presha), utasa na magonjwa yote kwa kutumia pipi hizi za upako,” anasema mchungaji huyo na kuongeza;
“Kila mgonjwa ninampa mbilimbili, moja kwa ajili ya kuponywa maradhi yote na ya pili ni ya mvuto wa biashara, kupendwa na utajiri wa Kimungu.”

Gazeti hili lilimweleza Nabii Bethania kwamba, mambo anayoyafanya kuanzia kukanyaga watu hadi kutumia jiwe na pipi kuponya ni upotoshaji wa watu na ni dalili za siku za mwisho ambapo alifunguka;
“Sijafuatwa na mtu yeyote kunilalamikia kwa sababu kanisa langu liko kihalali kabisa na mimi si mchungaji wa jina, bali nimesomea nchini Zambia.”

MAKANISA YENYE SHAKA
Kanisa hilo la Nabii Bethania ni miongoni mwa makanisa ambayo kila kukicha watu wanayatolea macho kwa vitendo visivyokubalika, lakini mwenyewe anadai kuwa ni kwa sababu hawahudhurii ibada na wengi wanapenda kuchafuliana majina.

Chanzo: Risasi Jumamosi

No comments